Beki Marcos Rojo huenda akafunguliwa mashtaka na chama cha soka nchini England (FA), kufuatia rafu aliomfanyia kiungo mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard, wakati wa mchezo wa robo fainali ya kombe la FA usiku wa kuamkia leo.
Beki huyo kutoka nchini Argentina, ameonekana akimkanyaga kwa makusudi Hazard sehemu ya ubavuni, baada ya kumkwatua kwa nyuma alipokuwa kwenye heka heka za kumkaba.
Hata hivyo, mwamuzi wa mchezo huo, Michael Oliver hakuliona tukio hilo jambo ambalo linatoa nafasi kwa FA kulichunguza kwa kina na kama wataona linapaswa kutolewa maelezo ni dhahiri watamfungulia mashtaka beki huyo.
Rojo alifanya tukio hilo ikiwa tayari Man Utd wapo pungufu, kufuatia kuadhibiwa kwa kiungo Ander Herera.
Endapo FA watajiridhisha kuhusu kosa hilo, Rojo huenda akafungiwa zaidi ya michezo mitatu, kama ilivyokuwa kwa beki wa Bournemouth, Tyrone Mings ambaye alimkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Man Utd, Zlatan Ibrahimovic.
Mings ameadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitano ambayo ipo chini ya chama cha soka nchini England (FA), baada ya kubainika alimkanyaga kwa makusudi Ibrahimovic.