Beki wa klabu ya Man Utd Marcos Rojo, amesema kikosi cha timu ya taifa ya Argentina hakitorejea kosa la kushindwa kutwaa ubingwa wa dunia, kama ilivyokua wakati wa fainali za mwaka 2014 nchini Brazil.

Rojo ambaye ni sehemu ya kikosi cha wachezaji 23 cha nchi hiyo ambacho kitakwenda Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia 2018, amesema kwa pamoja wachezaji wamejitathmini na kutafakari kwa kina, na kubaini kosa waliloifanya miaka minne iliyopita, hivyo hawatotaka lijirudie tena.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye tayari ameshaitumikia Argentina katika michezo 56, alikua sehemu ya wachezaji waliohisi uchungu wa kushindwa kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 2014, baada ya kufungwa na Ujerumani katika mchezo wa fainali bao moja kwa sifuri.

“Fainali za mwaka huu zina umuhimu mkubwa kwa Argentina, tumejihimiza sisi kama wachezaji kupambana kwa moyo wote, huku tukiamini hakuna anaeweza kutushinda tutakapokua uwanjani,” amesema Rojo kupitia tovuti ya Man Utd (http://www.manutd.com).

“Tunajivunia kuvaa jezi za timu ya taifa la Argentina, na hatupaswi kuwaangusha wananchi wanaotutegemea.”

“Tumeaminiwa na kupewa kila kitu kwa ajili ya kwenda Urusi kupambana, tutahakikisha hilo linafanyika tukiwa ndani na nje ya uwanja, hadi tukamilishe azma ya kutwaa ubingwa wa dunia.

“Tutafanya kila linalowezekana, ili tuwafurahishe mashabiki wetu.”

Kuhusu kupangwa na Nigeria katika kundi moja kwa mara nyingine tena, Rojo amesema huo ni mtihani mkubwa sana kwao, kwani wamekua wakiifunga timu hiyo kutoka Afrika kila wanapokutana nayo, lakini kwa mwaka huu wanajua hali itakua tofauti.

“Nafikiri hii itakua ni mara ya tatu ama ya nne tunakutanishwa na Nigeria, kwa hakika hautokua mchezo rahisi kwetu, maana kila mwaka tumekua tukishinda sisi, nao watahitaji kushinda, hivyo tunapaswa kuweka mazingira ya kuzuia mipango yao,”

“Kila mmoja anauchukulia tofauti mchezo huo, lakini kwa upande wetu tupo tayari kupambana na kupata matokeo mazuri.”

Timu nyingine zilizopangwa na Argentina katika kundi D ni Croatia na Iceland, ambazo pia Rojo anaamini zitawapa upinzani mkali, japo ameendelea kusisitiza timu yao itakua na nafasi ya kufuzu kwenda hatua ya makundi.

Argentina wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa dunia 2018, kwa kucheza dhidi ya Iceland Juni 16, kisha watapapatuana na Croatia Juni 21 na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi watakutanana Nigeria Juni 26.

Ryan Fredericks aikacha Fulham na kutimkia West Ham Utd
Video: Huu ni ukatili, huwezi kumuua mwenzio kwa wivu wa mapenzi- Dkt. Bisimba