Viongozi wa Manchester United wanaimani mshambuliaji wake, Marcus Rashford atasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Rashford ataingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake wakati wa majira ya kiangazi na kama hatawafikia muafaka basi mshambuliaji huyo anaweza kuondoka kwenye klabu hiyo akiwa mchezaji huru mwaka 2024.
Lakini Meneja wa klabu hiyo, Erik Ten Hag anaamini hilo haliwezi kutokea na kwamba mazungumzo baina ya pande hizo mbili yatafanya Rashford asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.
“Marcus anataka kubaki na tunataka abaki, hivyo nadhani tutafikia makubaliano ya pande zote mbili,” amesema Ten’Hag
United wamepiga hatua katika baadhi ya majadiliano ya kuongeza mkataba na nyota wake na ilitangaza kwamba beki wake wa kushoto, Luke Shaw alisainí mkataba mpya mwezi uliopita kabla ya mlinzi huyo wa kimataifa wa England hajafika mwaka wa mwisho wa mkataba wake.
Ten Hag amesema anajua kwanini klabu hiyo mpaka sasa haijafikia makubaliano na Rashford, ambaye ameifungia timu hiyo mabao 29 msimu huu, lakini alisisitiza ahusiki na kuchelewa huko.
“Ndio, najua ni kwanini lakini sitazungumzia mchakato huo,” ameongeza.
“Acha mchakato uendelee. Kwa sasa hili sio muhimu kwangu mimi au kwa Rashy.
Kwake anataka kufunga mabao zaidi msimu huu na amekuwa na msimu mzuri na timu imekuwa na msimu mzuri. Tunatakiwa kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa na kuweka mkazo huko.”
United inahitaji kushinda michezo yake miwili zilizosalia kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.