Rais wa Marekani Donald Trump ameishambulia China kwa jinsi ilivyoshughulikia kizembe mlipuko wa virusi vya corona (Covid 19) ambapo amesema janga hilo limekuwa na madhara makubwa kwa Marekani.
Kwa mujibu wa DW Rais Trump amesema corona imeiathiri Marekani kwa kiwango kikubwa kuliko mashambulizi ya mabomu dhidi ya kambi ya kijeshi ya Pearl Harbor ya mwaka 1941 au tukio la kigaidi la September 11.
Yatakumbukwa mashambulizi ya Japani kwenye kambi ya Pearl Harbor, Hawaii ambayo yalilazimisha Marekani kuingia katika vita ya pili ya dunia, na mkasa wa September 11 uliwaua Wamarekani zaidi ya 3,000 na kuisukuma Washington kuanzisha operesheni dhidi ya ugaidi
Aidha amesema kuwa ugonjwa wa Covid 19 ni moja ya matukio makubwa ambayo yamesababisha athari kubwa katika historia ya Marekani.
Hata hivyo Rais Trump ameilaumu China akisema virusi vya corona visingesababisha athari kubwa iwapo China ingefanikiwa kuvidhibiti kikamilifu vilipoanza tu mwishoni mwa mwaka jana.