Ikulu ya Marekani imesema inatarajia kufanya mazungumzo ya siku mbili kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu ndani ya ndege maalumu ya rais ikielekea jimbo la Florida, msemaji wa White House, Sarah Huckabee Sanders amesema majadiliano kati ya viongozi hao wawili yatalenga zaidi juu ya maandalizi kwa mazungumzo na Korea kaskazini pamoja na majadiliano mengi juu ya biashara.
Rais Trump na Abe wanafahamiana. Waziri Mkuu wa Japan ni kiongozi wa kigeni ambaye Rais wa Marekani amekutana naye pamoja na kuzungumza naye mara nyingi wakati wa urais wake.
Msemaji wa White House amesema Trump na Abe wana wasiwasi kuhusu Korea kaskazini ambayo ina programu za makombora na silaha za nyuklia ikikaidi vikwazo vya kimataifa.