Nchi ya Marekani, Uingereza na Australia zimetangaza kuwa zitabuni ushirikiano wa kiusalama katika eneo la Indo-Pasifiki utakaojumuisha kuisaidia Australia kupata manuwari zitakazokuwa zinatumia nguvu za nyuklia.
Ushirikiano huo umetangazwa na Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison.
Katika tangazo lililotolewa na viongozi hao kwa wakati mmoja kupitia njia ya video kutoka miji mikuu ya nchi zao, viongozi hao wamesisitiza kwamba Australia itakuwa haiweki silaha za nyuklia bali itakuwa inatumia mifumo inayoendeshwa na nyuklia kwa ajili ya manowari hizo, kwa ajili ya kujilinda kutokana na vitisho vya siku zijazo.
Johnson amesema ni uamuzi muhimu wa Australia kupata teknolojia hiyo kwani itaufanya ulimwengu kuwa salama.
Waziri Mkuu wa Australia Morrison amesema manowari hizo zitatengenezwa katika mji wa pwani ya Australia wa Adelaide kwa ushirikiano wa karibu na Marekani na Uingereza.
Haya yote yanajiri wakati ambapo ushawishi wa China katika eneo hilo ukiwa unaongezeka.