Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani, Rex Tillerson wamekutana kwaajili ya kufanya mazungumzo ya kutafutia ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza baina ya mataifa hayo.
Katika mazungumzo hayo, Urusi imesema kuwa inamatumaini makubwa kuwa Marekani itakuwa tayari kuendeleza mazungumzo kuhusu masuala magumu licha ya mvutano mkali uliojitokeza kati ya nchi hizo.
Aidha, Sergei Lavrov amesema kuwa Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu Urusi kulipiza kisasi dhidi ya hatua ilizochukua za kuiwekea vikwazo nchi hiyo kitu ambacho amesema sio cha kweli.
Mazungumzo hayo ni ya kwanza tangu Rais wa Marekani, Donald Trump kusaini sheria ya kuiwekea vikwazo Urusi, kitu ambacho kilipingwa vikali na Urusi huku ikisema vikwazo hivyo vinahatarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo.
Hata hivyo, katika mazungumzo hayo ya kutafuta ufumbuzi wa tofauti zilizojitokeza baina ya nchi hizo, pia walijadili suala la mpango wa majaribio ya makombora ya masafa marefu unaofanywa na Korea Kaskazini.