Mshambuliaji kutoka nchini Chile, Alexis Alejandro Sánchez amEachwa kwenye kikosi cha Man Utd kilichosafiri kuelekea nchini Marekani, kwa ajili ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Sanchez amelazimika kuachwa kwenye safari hiyo baada ya kukosa kibali cha kuingia nchini Marekani (VISA), kufuatia kikwazo cha hukumu iliyomfika mapema mwaka huu huko Hispania.
Mshambuliaji huyo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi minne jela (Miezi 16) ama kulipa faini, baada ya kukutwa na makosa ya kukwepa kodi wakati wote alipokua akiitumikia FC Barcelona kuanzia mwaka 2011-14.
Hata hivyo, uongozi wa Man Utd unaendelea kushughulikia suala la VISA ya mshambuliaji huyo, huku kukiwa na matumaini makubwa ya kufanikisha siku za karibuni.
Kwa sheria za Marekani, ni vigumu kwa mtu yoyote aliyewahi kuhukumiwa mahakamani hususan masuala ya ukwepaji kodi, kupata kibali cha kuingia nchini kwao.
Mchezaji mwingine ambaye hajaambatana na kikosi cha Manchester Utd kwenye ziara hiyo ni beki/kiungo kutoka nchini Uholanzi, Daley Blind ambaye anatarajia kukamilisha uhamisho wa kurejea Ajax kwa pauni milioni 14.1.
Wengine ni Paul Pogba, Romelu Lukaku, Marouane Fellaini, David de Gea, Marcus Rashford na Jesse Lingard ambao watajiunga na kambi ya maandalizi ya msimu mpya Agosti 6, baada ya kumaliza likizo ya mapumziko.
Wachezaji hao wamepata nafasi hiyo, baada ya kumaliza majukumu ya kuzitumikia timu zao za taifa kwenye fainali za kombe la dunia zilizomalizika nchini Urusi mwishoni mwa juma lililopita.
Kikosi cha Man Utd kikiwa nchini Marekani kitacheza michezo mitano ya kirafiki huku kikiweka kambi katika miji ya California, Phoenix na Arizona.
Katika michezo hiyo mitano ya kirafiki wababe hao wa Old Trafford watapambana na mahasimu wao kutoka England, Liverpool, mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid pamoja na AC Milan.