Serikali ya Marekani imeinyooshea kidole China kuwa inajaribu kuiibia utafiti wa dawa ya virusi vipya vya corona (covid-19) kwa kufanya udukuzi.
Imeeleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na mashambulizi mengi ya udukuzi dhidi ya Marekani hususan kwenye taasisi za afya zinazofanya utafiti wa dawa ya kinga dhidi covid-19.
Maafisa wa Serikali wamekaririwa na CNN wakieleza kuwa hospitali, maabara na makampuni ya dawa yote yamedukuliwa. Imeeleza kuwa Idara ya Afya na Huduma za Binadamu ambayo inasimamia Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa na Kinga kimekuwa kikishambuliwa na wadukuzi kila siku.
“Ni salama kusema kuwa kuna sehemu mbili tu duniani ambapo wanaweza kushambulia Idara ya Afya na Huduma za Binadamu kwa namna wanavyoshambulia sasa,” afisa wa Serikali anayehusika na idara hiyo amekaririwa na CNN bila kutaja jina lake.
Amefafanua kuwa kutokana na ukubwa wa mashabulizi hayo, China na Urusi ndio nchi pekee zinazoweza kuhusika.
Hata hivyo, alieleza kuwa China ndio nchi inayokuwa ya kwanza kutuhumiwa kwa mashambulizi hayo kutokana na uhusiano wake na Marekani kwa sasa.
Idara ya Sheria na Haki ya Marekani pia imeweka msisitizo kuwa China ni watuhumiwa namba moja wa mashambulizi hayo ya udukuzi.
“Hilo ndilo linaweza kuwa hitimisho la hayo yote yanayosemwa… tunafuatilia kwa karibu ongezeko la mashambulizi ya mtandaoni katika vituo vyetu vya tiba, utafiti, vyuo vikuu na kila anayefanya utafiti katika eneo hili,” John Demers, Mkuu wa Idara ya Sheria na Haki kilicho ndani ya Idara Kuu ya Usalama wa Taifa alijibu alipoulizwa na CNN kuhusu tuhuma dhidi ya China.
“Hakuna kitu chenye thamani leo zaidi ya utatifi wa kibailojia unaohusu tiba au kinga ya virusi vya corona. Ni muhimu sana sio tu kwa thamani ya kibiashara lakini pia nchi yoyote, kampuni au maabara yoyote ya utafiti ambayo itakuwa ya kwanza kutengeneza dawa itakuwa na simulizi la mafanikio makubwa,” aliongeza Demers.
Katika siku za hivi karibuni, Marekani na China zimekuwa zikishutumiana kuhusu virusi vya corona, kila mmoja akimtupia lawama mwenzake kwa madai kuwa yeye ndiye chanzo cha kusambaa kwa virusi hivyo.
Wiki hii kulikuwa na ripoti kuwa uongozi wa jimbo la Missouri la Marekani limefungua mashtaka dhidi ya Serikali ya China kwa madai kuwa haikufanya jitihada za kutosha kudhibiti kusambaa kwa Covid-19.