Serikali ya Marekani imesema kuwa Iran inatakiwa kuchukuliwa hatua mapema kwani isipochukuliwa hatua mapema inaweza kuwa kama Korea Kaskazini kwa kuzalisha silaha za nyuklia.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amesema Iran inafanya uchokozi wa hali ya juu na inanuia kuvuruga uthabiti katika Mashariki ya Kati na kuhujumu juhudi za Marekani katika kanda hiyo.
“Iran isipochukuliwa hatua inaweza kuwa kama Korea Kaskazini na kuubeba ulimwengu wote katika safari hiyo,” amesema Tillerson.
Aidha, Rais Donald Trump kufuatia hayo, tayari ameagiza utathmini mpya ufanywe kuhusu mkataba uliotiwa saini kati ya nchi za Magharibi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo mapoja na hayo yoye, Iran hadi kufikia sasa haijasema lolote kuhusu tamko hilo jipya kutoka kwa Marekani.
Kabla ya tuhuma hizo mpya, Iran imewa ikikanusha mara kwa mara tuhuma kutoka kwa nchi za Magharibi kwamba inajaribu kustawisha silaha za nyuklia.
Tillerson amesema utathmini huo mpya kuhusu Iran, ambao aliutangaza katika Bunge la Congress, amesema utatathmini iwapo Tehran imetimiza makubaliano ya mkataba huo wa nyuklia pia utachunguza vitendo vya Iran Mashariki ya Kati.
Hivi karibuni Marekani imeionya Korea Kaskazini na kusema taifa hilo linajaribu kufanya uchokozi wa kivita baada ya nchi hiyo kufanya jaribio la kombora ambalo halikufanikiwa.
Korea Kaskazini ilijibu tuhuma za Marekani ambapo imeeleza kuwa inaweza kufanya majaribio ya makombora kila wiki na kuionya Marekani kwamba itaikabili kwa vita vikali iwapo itathubutu kuishambulia kijeshi.