Marekani imesema kuwa itaendelea kutekeleza vikwazo ilivyopitisha Novemba 22, 2015 dhidi ya Burundi kutokana na kuendelea kwa hali ya taharuki, ikiwemo uvunjifu wa amani nchini humo.
Imesema kuwa ili kukabiliana na tishio hilo vikwazo hivyo vilivyokuwa vimewekwa lazima viendelezwe baada ya Novemba 22, 2018.
Aidha, hali ya usalama nchini Burundi inaendelea kuwa siyo ya kawaida na ni tishio kwa usalama wa taifa na sera ya nje ya Marekani inayotokana na hali halisi nchini Burundi, imesema taarifa ya Ikulu ya Marekani iliyotolewa na Rais Donald Trump
Agizo la Trump limesema kuwa kumekuwepo na uvunjaji wa amani dhidi ya raia, ghasia, uchochezi unaopelekea vurugu, na ukandamizaji mkubwa wa kisiasa, ambao unahatarisha amani, usalama, na utulivu wa Burundi na eneo lote.
“Hivyo, kwa mujibu wa kifungu 202(d) ya Sheria ya Dharura ya Kitaifa (50 U.S.C 1622 (d), mimi naendeleza tamko hilo la dharura la amri ya kiutendaji.”ameandika Trump
Hata hivyo, wakati wa uongozi wa Rais Obama’ alisaini amri ya kiutendaji iliyotangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa Burundi na rasilimali zao kufuatia uvunjaji wa amani dhidi ya raia, ghasia, uchochezi uliopelekea vurugu, na ukandamizaji mkubwa wa kisiasa, ambao ulikuwa unahatarisha amani, usalama, na utulivu wa Burundi na eneo lote.