Marekani imeikaribisha Korea Kaskazini kwenye meza ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa silaha za nyuklia uliovuruga mahusiano kati ya nchi hizo na washirika wake.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema kuwa kupata suluhu ya mgogoro huo, wanapaswa kukutana na kufanya mazungumzo.
“Tukutane na tuzungumze kuhusu hali ya hewa inayoendelea kama mnataka, na tuzungumze kama itakuwa ni mazungumzo ya aina gani, kama ndicho kinachotakiwa,” alisema.
Hata hivyo, alitoa sharti kwa Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya silaha zake za nyuklia inayoendelea nayo kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Urusi na China ambao wameitaka Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya makombora yake na kukaribia kwenye meza ya mazungumzo.
Tillerson alizitaka Urusi na China kuishinikiza Korea Kaskazini kutii masharti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Balozi wa Korea Kaskazini, Ja Song Nam alisema kuwa uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini ulitengenezwa na Marekani kwa lengo la kuikwamisha nchi hiyo kuendelea na mpango wake wa kuimarisha vikosi vyake vya silaha za nyuklia.
Nchi hiyo haijazungumzia wito wa Marekani wa kukaa mezani kutafuta suluhu ya mgogoro huo.