Sudan imetakiwa kukata mara moja uhusiano wa kijeshi kati yake na Korea Kaskazini kama inataka kuondolewa kwenye orodha ya Marekani ya mataifa yanayofadhili ugaidi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, maafisa waandamizi wa Marekani wameitaka Sudan kuchukua hatua hiyo haraka kwani kuna taarifa za uhakika kuwa inapata msaada wa kijeshi kutoka Korea Kaskazini.
Ingawa mwaka jana Marekani ililegeza kamba kwa kuondoa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Sudan, bado imeendelea kuiweka katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi ikiwa ni pamoja na Syria, Iran na Korea Kaskazini.
Maafisa wa Sudan wamekana kuwa na ushirikiano wowote na Korea Kaskazini huku wakilalamika kuwa uchumi wa nchi hiyo unaporomoka kwani wawekezaji wanaogopa kuwekeza wakiamini kuwa nchi hiyo ina ushirikiano na makundi ya kigaidi.
“Sudan inawahakikishia kuwa haina uhusiano wowote na Jamhuri ya Watu wa Korea, katika ngazi yoyote ile,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan iliyotolewa Jumapili iliyopita.
Makombora mengine yashushwa Syria, Israel yatamba
Sudan imeendelea kuwa katika hali ngumu ya kiuchumi, ikishuhudia mfumuko mkubwa wa bei na ubovu wa maisha ya wananchi, hali iliyosababisha migomo.
Nchi hizo mbili hazijawahi kuwa na uhusiano wa Kidiplomasia kwa miaka mingi lakini makundi mbalimbali ya haki za binadamu na wanaharakati wanadai kuwa kuna uhusiano wa kijeshi kati yao.