Uongozi wa juu wa jeshi la Marekani umekiri kuwa wanajeshi kadhaa walijeruhiwa katika shambulio la makombora lililofanywa na Iran katika vituo viwili vya jeshi nchini Iraq mapema mwezi huu.
Msemaji wa uongozi wa jeshi la Marekani, Kapteni Bill Urban amesema kwamba ingawa hakuna mwanajeshi hata mmoja aliyeuawa katika shambulio la Iran la Januari 8 katika kituo cha jeshi la anga cha Al Assad, wako wengi waliopatiwa matibabu kutokana na matatizo ya kupumua kutokana na mripuko na bado wanaendelea na tathmini ya afya zao.
Urban alifafanua kuwa, ni utaratibu wa kawaida kwamba wanajeshi wote waliokuwapo katika eneo la shambulio wanachunguzwa kwa ajili ya kujua iwapo wamepata athari katika ubongo wao, na kama itaonekana lazima wanasafirishwa kwa matibabu zaidi ya juu.
Siku ya shambulio hilo, baadhi ya wanajeshi walisafirishwa kutoka kituo cha jeshi la anga cha Al Asad nchini Iraq kwenda katika kituo cha matibabu cha Landstuhl nchini Ujerumani, wakati wengine walipelekwa katika kambi ya Arifja nchini Kuwait kwa ajili ya uchunguzi.