Zikiwa zimesalia saa chache kukamilisha saa 72 alizozitoa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro kwa wanadiplomasia wa Marekani kuondoka nchini humo, Marekani imesema hawataondoka na kuonya kuwa endapo atawagusa ua kuwatisha watajibu ipasavyo.
Onyo hilo limetolewa na mshauri wa Ikulu ya Marekani, John Bolton ambaye ameeleza kuwa vitisho dhidi ya wanadiplomasia wao itakuwa ni kama ishara ya kuchimba kaburi la utawala wa sheria.
Marekani na nchi nyingine zaidi ya 20 zimeeleza kuwa zinamuunga mkono na kumtambua mpinzani wa Maduro, Juan Guaido kama Rais wa Mpito wa Venezuela.
Hata hivyo, nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Urusi, China, Uturuki, Cuba na washirika wao wamepinga hatua hiyo ya Marekani na kuahidi kumuunga mkono Maduro katika mgogoro huo.
Aidha, Maduro amefanya mahojiano na kituo cha habari cha Uturuki ambapo ameeleza kuwa kinachofanywa na Marekani ni kujaribu kuipindua Serikali yake halali, kwa kuwa hawapendi kuona nchi hiyo inakuwa kiuchumi ili wao waendelee kuwa juu yao.
Aliongeza kuwa nchi nyingi za Uingereza zinaisujudia Marekani ndio sababu zimejitokeza kumpinga.
“Nchi zote za Ulaya zinamsujudia Donald Trump (Rais wa Marekani). Ni rahisi hivyo, hususan linapokuja suala la Venezuela,” alisema Maduro alipohojiwa na vyombo vya habari vya Uturuki, na kukaririwa pia na CNN.
“Hii ndio sababu wanataka kufanya mapinduzi. Hawataki tuendelee. Wanataka kuvamia na kuhujumu mifumo yetu ya uchumi,” aliongeza.
Hata hivyo, Maduro alieleza kuwa amekuwa akimtumia jumbe nyingi Rais Trump lakini hazijibu, akadai anaamini hilo linatokana na kuelemewa na matatizo ya ndani ya Marekani.
Maelfu ya wafuasi wa Guaido wameingia mtaani wakipinga Serikali ya Maduro huku kiongozi huyo wa upinzani ambaye ni Mkuu wa Bunge la Taifa akijitangaza kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yalizuka mwezi mmoja baada ya Maduro kuapishwa kuwa Rais kwa kipindi cha pili, kufuatia uchaguzi uliofanyika Mei mwaka jana ambao wapinzani wake wanaupinga wakidai uligubikwa na wizi wa kura.