Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken amemtaka Rais wa Rwanda, Paul Kagame kuacha kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi la waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, huku akitoa mwito kwa nchi hizo mbili kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi uliopita nchini Angola..
Blinken ameyasema hayo na kuonesha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa umwagaji damu huku Msemaji wa wizara hiyo, Ned Price alisema Blinken alizungumza kwa njia ya simu na kiongozi huyo wa Rwanda.
Ameeleza kuwa Blinken alimuambia Kgame juu ya kwamba hatua yoyote ya nje ya kuyaunga mkono makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapaswa kusitishwa, ikiwemo uungaji mkono kutoka Rwanda kwa kundi la M23.
Aidha, amesema Blinken pia alilaani kuzuka tena kwa matamshi ya chuki na kauli za uchochezi zinazotolewa hadharani zikiilenga Rwanda na kukumbusha athari za kutisha za kauli kama hizo, zilizoshuhudiwa mwaka 1994 katika vita vya kimbari vilivyowalenga watu jamii ya kabila la Watutsi.