Marekani imenunua kiasi chote cha dawa iliyothibitishwa kuwasaidia wagonjwa wa virusi vipya vya corona kupona haraka, iliyopewa jina la remdesivir.
Dawa hizo zinazotengenezwa na Kampuni ya Gilead, zimetajwa kuuzwa kwa $533 kwa dozi moja (sawa na Sh 1,235,000) za Tanzania), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali ya Marekani. Hivyo, dozi sita ni $3,200.
Marekani imenunua mzigo wote utakaozalishwa na kampuni hiyo katika kipindi cha Julai, Agosti na Septemba, hali inayoipa ugumu nchi nyingine yoyote kununua dawa hiyo kwa sasa.
“Serikali ya Rais Trump inawamudu wasambazaji wa remdesivir na imejipanga kununua dawa zote za miezi mitatu kwa ajili ya wananchi wake. Hivyo, hakutakuwa na kitu kwa ajili ya Ulaya na nchi nyingine duniani hadi hapo baadaye,” Dkt. Andrew Hill, Mtaalam Mwandamizi wa Utafiti wa Chuo Kikuu cha Liverpool amekaririwa na The Guardian.
Marekani imenunua zaidi ya dozi 500,000 ambazo ni zaidi ya asilimia 90 ya kiasi chote kinachozalishwa na kampuni hiyo kwa miezi mitatu kuanzia leo. Dawa hizo zilizokuwa za kwanza kupata uthibitisho, awali zilikuwa zimetengenezwa kutibu Ebola lakini hazikufanikiwa.
“Marekani inataka kuhakikisha kwamba kila raia wake anayetaka kupata dawa hizo anazipata. Serikali ya Trump inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inaendelea kujifunza kuhusu dawa hizo, na kuifaidisha zaidi Marekani kwanza kwakuwa ndiyo nchi iliyoathirika zaidi,” Katibu Mkuu wa Afya na Huduma za Kibinadamu wa Marekani amekaririwa.
Taifa hilo limerekodi zaidi ya visa milioni 2.6 vya corona na vifo zaidi ya 129,000, na watu 826 waliokuwa wameathirika wamepona.
Baadhi ya majimbo ambayo yalikuwa yamelegeza masharti ya ‘lockdown’, yamerejesha tena masharti hayo baada ya kushuhudia ongezeko la kasi la visa vya corona.
Jumatatu wiki hii, Serikali ya Arizona iliamuru bar, kumbi la sinema, majumba ya mazoezi (gyms) na sehemu nyingine za starehe kufungwa tena kwa kipindi cha mwezi mmoja. Texas, Florida na California wamerejesha tena masharti baada ya kulegeza kwa muda.
Mwenyekiti wa CCM Ubaruku auawa kwa shoka kitandani