Viongozi kutoka vyama vyote katika bunge la Marekani wamekubaliana kuhusu sheria ambayo inaruhusu vikwazo vipya kuiadhibu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani uliofanyika mwaka jana.
Sheria hiyo pia imelenga kumpunguzia madaraka Rais wa sasa wa nchi hiyo, Donald Trump wa kuipunguzia au kuiondolea vikwazo Urusi ambayo imebainika kuingilia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Urusi bado inashikilia msimamo wake wa kutoingilia uchaguzi huo wala kutenda baya lolote, lakini uchunguzi ambao umefanywa na Marekani unatathmini ikiwa yeyote katika kampeni ya Trump alishirikiana na maafisa wa Urusi
Hata hivyo, kama Sheria hiyo itapitishwa basi itaruhusu kuwekwa kwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi kwa kulimega eneo la Crimea mwaka 2014 na madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani