Marekani imeanzisha mashambulizi dhidi ya mifumo ya kompyuta ya Iran, saa chache tangu Rais Trump atangaze kusitisha mpango wa kufanya mashambulizi ya anga kwenye nchi hiyo.
Kwa mujibu wa New York Times, mashambulizi hayo ya kimfumo yamefanikiwa kuharibu mifumo ya kufyatulia makombora na baadhi ya ndege zisizo na rubani za Iran.
Marekani imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya majibu ya kitendo cha Iran kutungua ndege yake isiyo na rubani.
Hata hivyo, hakuna chanzo chochote huru ambacho kimethibitisha madhara yatokanayo na mashambulizi hayo dhidi ya mifumo ya Iran.
Rais Donald Trump amesema kuwa watahakikisha Iran haitengenezi silaha za kinyuklia na kwamba itaendelea kuiwekea vikwazo vya kiuchumi hadi itakapoahirisha mpango wake.
Taharuki kati ya nchi hizo mbili iliibuka mwaka 2015 baada ya Marekani kutangaza kuachana na mpango wa nyuklia ambao Iran ilisaini pamoja na mataifa yenye nguvu duniani. Mpango huo uliratibiwa na Barack Obama aliyekuwa Rais wa Marekani wakati wa makubaliano hayo.
Trump alikosoa hatua ya Obama kuingia makubaliano hayo na Iran akieleza kuwa lilikuwa kosa kubwa kuwahi kufanyika. Rais huyo alieleza kuwa ataendelea kuishinikiza Iran kwa kutumia vikwazo vya kiuchumi bila kuwabembeleza na kwamba watahakikisha hawatengenezi silaha za kinyuklia.
Iran imelaani kitendo cha Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo na kuendelea kuiwekea vikwazo na imeeleza kuwa itaendelea kutengeneza nyuklia zaidi ya kiwango walichokubaliana.
Juzi, Iran ilieleza kuwa iliitungua ndege ya Marekani kwa sababu iliingia kwenye anga lake na kwamba itaendelea kujilinda ingawa haina nia ya kuingia vitani dhidi ya nchi yoyote. Marekani nayo imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa ndege hiyoisiyo na rubani ilikuwa kwenye anga la Kimataifa.
Taharuki kati ya nchi hizo inatarajiwa kujadiliwa Jumatatu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya Marekani kueleza kuwa itaomba kuitishwa mkutano wa dharura kuijadili Iran.
Wakati huohuo, Iran nayo imeeleza kuwa itaishtaki Marekani kwenye Baraza hilo kutokana na kukiuka sheria za kimataifa.