Marekani imeshusha rungu la vikwazo kwa jeshi la China kufuatia hatua ya jeshi hilo kununua ndege za kivita na makombora kutoka Urusi.
Marekani imeeleza kuwa imefikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa kitendo cha China kinakiuka masharti ya vikwazo dhidi ya Urusi. Imeelezwa kuwa vikwazo hivyo dhidi ya Urusi viliwekwa kutokana na vitendo vya taifa hilo nchini Ukraine pamoja na kuingilia uchaguzi wa Marekani.
China imeripotiwa kununua ndege 10 za kijeshi za Urusi aina ya Sukhoi Su-35 (pichani) na makombora aina ya S-400. China haijawahi kuunga mkono hatua za Marekani kuiwekea vikwazo Urusi tangu mwaka 2014.
Marekani inaituhumu China kwa kuingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 uliompa ushindi Donald Trump. Hata hivyo, Urusi imekuwa ikikanusha vikali tuhuma hizo dhidi yake.
Mataifa hayo yenye nguvu pia yamekuwa yakipishana katika suala la vita vya Syria pamoja na mgogoro wa kinyuklia katika Rasi ya Korea.
Rais Donald Trump alitia sahihi kwenye hati ya vikwazo hivyo Alhamisi wiki hii ambapo mlengwa amedaiwa kuwa Urusi na wote wanaojihusisha naye.
“Mlengwa mkuu katika vikwazo hivi ni Urusi. Vikwazo hivi havilengi kushusha heshima ya uwezo wa ulinzi wa nchi yeyote. Lakini vimelenga katika kuifanya Urusi ilipe gharama kwa vitendo vyake,” afisa Mwandamizi wa Marekani amekaririwa na BBC.
Hata hivyo, mbunge wa Urusi, Franz Klintsevich ameviambia vyombo vya habari kuwa vikwazo vya Marekani haviwezi kuzuia Urusi kuuza ndege zake za kivita na makombora.
Ripoti ya hivi karibuni ya ‘Chatham House’ imeeleza kuwa India, China na Vietnam ndio wateja wakuu zaidi wa silaha za Urusi.