Marekani imesema imetoa mapipa Milioni 30 ya mafuta kutoka kwenye hifadhi yake ya kimkakati ya mafuta ikiwa ni sehemu ya mpango wa muungano wa Nchi 30 ambazo zimekubaliana kutoa mapipa Milioni 60 ya mafuta kutoka kwenye hifadhi zake kote ulimwenguni ili kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta Duniani.

Mpango huu wa muungano wa nchi 30 kutoa mafuta unakuja baada ya mzozo wa Ukraine na Urusi ambao mpaka sasa umesabisha bei za mafuta kupanda katika nchi nyingi duniani.

“Tuko tayari kufanya zaidi ikibidi, tukiwa na umoja na washirika wetu, hatua hizi zitasaidia bei butu ya gesi hapa nyumbani na najua habari kuhusu kinachoendelea inaweza kuonekana kuwa ya kutisha lakini nataka mjue kuwa tutakuwa sawa,” imesema Marekani.

Bei ya mafuta ghafi kwenye Bara la Ulaya sasa imefikia dola 105 na senti 79 kwa pipa, inafahamika kwenye Nchi zinazozalisha mafuta duniani Urusi ni Mzalishaji muhimu baada ya Saudi Arabia miongoni mwa nchi za shirika la wauzaji mafuta la OPEC.

Nchini Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta hapa nchini ambapo bei za rejareja na jumla za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es salaam zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la February 2, 2022 ambapo kwa mwezi March bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Tsh. 60 kwa Lita ( sawa na 2.42%) na Tsh. 65 kwa lita (sawa na 2.77%) na mafuta ya taa imepungua kwa Tsh. 83 kwa lita (sawa na 3.63%).

EWURA imesema kuwa bei hizi zingeweza kuwa juu zaidi kama Serikali isingechukua hatua ya kuahirisha tozo ya Tsh. 100 kwa lita kwenye bidhaa za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa.

Imeelezwa kuwa mabadiilko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika Soko la Dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya Kimarekani.

Wiki iliyopita bei ya mafuta ilipanda na kuvuka dola mia moja kwa mara ya kwanza tangu miaka saba iliyopita ambapo ongezeko hili linatajwa kusababishwa na hofu, baada ya Mzalishaji mkubwa wa mafuta Urusi kufanya mashambulio nchini Ukraine.

Taharuki ya ugaidi yasitisha shughuli za mahakama Nchini Kenya
Meli iliyobeba magari ya kifahari 4,000 yazama