Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright, amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo.

Dkt. Wright amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi jijini Dar es Salaam ambapo amejadili masuala ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Marekani.

Katika mazungumzo ya viongozi hao, Profesa Kabudi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, wamegusia harakati za kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini.

Profesa Kabudi amemhakikishia Balozi Dkt. Wright kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza hususani katika sekta za utalii,kilimo na biashara na kumhakikishia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru,haki na wa amani.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika sekta ya utalii serikali ya awamu ya tano imedhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili .

Kwa upande wake Balozi Dkt. Donald Wright amemhakikishia Waziri kabudi kuwa atahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika sekta za kilimo, biashara, huduma za afya na viwanda pamoja na kuhamasisha watalii kutoka marekani kuja nchini.

“Natumia pia fursa hii kuwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora kutekeleza malengo yao kimaendeleo,” amesema Dkt. Wright. 

 

Tanzania kuanza kusafirisha nje mbegu asili za mboga
Balozi apongeza usimamizi wa sheria ya usalama kazini