Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na Klabu ya Manchester United, Anthony Martial amesema hakukataa kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa mwishoni mwa juma lililopita.
Manchester United ililazimishwa sare ya 2-2 ugenini (Villa Park), baada ya kuongoza kwa mabao mawili kwa dakika 79, lakini wenyeji walisawazisha na kupata alama moja nyumbani.
Baada ya mchezo huo Meneja wa Muda wa Manchester United Ralf Rangnick aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Martial aligoma kuingia Uwanjani baada ya kumuaru kufanya hivyo.
Martial amejibu tuhuma hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika: “Kamwe sijakataa kuichezea Man United, nimekuwa hapa kwa miaka saba, sitavunja heshima hiyo na sitaivunjia heshima klabu na mashabiki,”
Martial anahitaji kuondoka kwenye Dirisha Dogo la Usajili mwezi huu Januari, huku akiwa hajajumuishwa kwenye kikosi tangu Desemba 2, mwaka jana kwenye mchezo wake wa mwisho ambao Man United walishinda 3-2.
Martial anatumai kuwa dirisha hili atatolewa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, huku timu ya Sevilla ikiwa ndio chaguo la pekee ingawa Barcelona na Juventus nao wanahitaji huduma yake.