Kiungo wa Arsenal Martin Odegaard amekiri Arsenal inahitaji kuimarika zaidi baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves, juzi Jumamosi (Desemba 02).
Arsenal walipata faida ya mabao 2-0 pale kwenye Uwanja wa Emirates, huku Bukayo Saka na Odegaard kila mmoja akifunga bao ndani ya dakiká 15.
Hata hivyo, ‘Washika Bunduki’ hao waliwaruhusu Wolves kurejea mchezoni wakati walipofunga bao zikiwa zimesalia dakika nne za muda wa kawaida.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Norway, Odegaard amesisitiza kuwa Arsenal lazima wafanye vizuri zaidi wanapokuwa kwenye uongozi bora.
Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 24. alisema: “Tulianza tena kwa nguvu sana. Kipindi cha kwanza klikuwa kizuri. Tulifunga mabao mawili mazuri na kutawala kila kitu.
“Tumewaruhusu waingie kidogo tukiwa na bao, lakini huo ni mpira wa miguu. Nadhani tunapaswa kujifunza kutokana na hilo.
“Tunajua kwenye Ligi Kuu huwezi kamwe kuzima mchezo. Leo ulikuwa mfano mzuri wa hilo. Lazima tuhakikishe tunafanya vema zaidi wakati ujao tukiwa 2-0.”
Lakini licha ya kukosolewa kwa kukosa umakini, Odegaard alifurahishwa na kiwango cha Arsenal.
Aliongeza: “Imekuwa wiki nzuri na matokeo mazuri. Tupo kileleni na lazima tuzidi kuimarika na kuendelea kusonga mbele.
“Ratiba ni ngumu, lakini karibu msimu mzima ni mgumu. Huna muda mwingi wa kupona.
“Lazima tuwe wajanja katika kupona na kupumzika kabla ya mchezo unaofuata dhidi ya Luton.”
Ushindi dhidi ya Wolves unamaanisha kuwa Arsenal wako kileleni mwa jedwali mwa msimano kwa pointi nne, huku safari ya kuelekea Luton ikitarajiwa Jumanne.