Klabu ya Arsenal inakaribia kuingia mkataba mpya na nahodha wake, Martin Odegaard, vyanzo vya habari vimeeleza.
Mazungumzo kwa sasa yako katika hatua kubwa kuhusu mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 200,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 620) kwa juma, ikiwa ni sawa na Pauni milioni 40 (sawa na Sh bilioni 123) kwa urefu wa mkataba wenyewe, Odegaard anatarajia kumwaga wino juma hili.
Mchezaji huyo amebakisha miaka miwili katika mkataba wake wa sasa na Arsenal, ambao una thamani ya kiasi cha Pauni 115,000 (sawa na Sh milioni 356) kwa juma.
Malipo ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Norway yanatarajia kuongezeka katika klabu hiyo yeye maskani yake kwenye Uwanja wa Emirates, huku kocha Mikel Arteta akisema kuwa nyota huyo mbunifu yupo katika mipango yake.
Inaaminika kuwa Arsenal imemthaminisha Odegaard kwa zaidi ya Pauni milioni 100 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 309).
Anatarajia kuungana na wachezaji kama akina William Saliba, Bukayo Saka na Gabriel Martinelli waliojifunga kuichezea timu ya London kwa muda mrefu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alifanywa kuwa nahodha mpya wa Arsenal baada ya kuondoka kwa Pierre Emerick Aubameyang Januari mwaka 2022.
Odegaard pia anatarajia kuingoza timu ya Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya PSV keshokutwa Jumatano (Septemba 20), ukiwa ni mchezo wao wa kwanza katika mashindano hayo baada ya miaka sita.
Alijiunga na klabu hiyo kwa mkopo wa muda mfupi akitokea Real Madrid Januari mwaka 2021.