Seneta wa Nairobi nchini Kenya, Mike Sonko ametetea uamuzi wa Serikali kupiga marufuku daladala kuingia katikati ya jiji, akidai kuwa itasaidia watu kufanya mazoezi kuimarisha afya zao.
Mamia ya wananchi leo wamelazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu jijini humo, baada ya daladala maarufu kama ‘matatu’ kuishia katika vituo vipya, mbali kidogo na vituo vya katikati ya jiji kama walivyoelekezwa na Serikali.
Akizungumza mapema leo, Gavana Sonko amesema kutokana na hali hiyo hivi sasa wananchi wengi wataokoa fedha nyingi walizokuwa wanatumia kwenda kwenye vituo maalum vya mazoezi (gym), na kuwasaidia wale ambao hawakuwahi kwenda gym.
“Kutoka Muthurwa hadi CBD ni mwendo wa dakika moja kwa kutembea kwa miguu. Watu wengi huwa hawaendi kwenye vituo vya mazoezi. Tunahitaji sana nyie wananchi mfanye mazoezi,” alisema Sonko.
Aliongeza kuwa amezungumza na Rais Uhuru Kenyatta kwa njia ya simu na amekubali kuwa ataleta mabasi maalum kwa ajili ya kuwabeba watu wenye ulemavu wanaposhushwa katika vituo vipya vya matatu.
Serikali imeeleza kuwa imelazimika kuzuia matatu kuingia katikati ya jiji ili kupunguza msongamano mkubwa. Takribani magari 20,000 aina ya matatu hufanya kazi zake ndani ya jiji hilo.
Hata hivyo, wananchi wengi wamelalamikia kitendo hicho wakidai kuwa mwendo wanaotembea ni mrefu na kwamba utasababisha washindwe kuwahi makazini.
Marufuku hiyo imekumba pia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na bajaji.