Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa jana alitangaza kuwa Serikali inarudisha marufuku iliyokuwepo ya uuzaji wa pombe na zuio la kutotoka ndani usiku ili kukabili maambukizi ya Corona.
Rais Ramaphosa amesema marufuku hiyo ya kutotoka ndani usiku itaanza kutekelezwa leo, Julai 13, 2020 na itakuwa ikianza saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri kila siku.
Nchi hiyo iliweka masharti makali mnamo mwezi Machi, hatua iliyochangia kupungua maambukizi lakini baadaye Rais huyo alitangaza kulegezwa kwa baadhi ya masharti, kufuatia hofu kubwa ya kudhoofika kabisa kwa uchumi wa Taifa hilo.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirka la Afya Duniani (WHO) Afrika Kusini ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya maambukizi barani Afrika, na ni mojawapo kati ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya kila siku duniani.
Kumekuwa na jitihada za kupunguza misongamano ya wagonjwa kwenye Hospitali, hali inayowanyima nafasi za matibabu watu wenye maambukizi ya corona wanaoendelea kuongezeka kila siku.
Afrika Kusini hadi kufikia leo ina jumla ya Waathirika 276,242, Wagonjwa waliopona ni 134,874 na vifo vimefikia 4,079.