Wapinzani wa Young Africans katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Marumo Gallants wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Jumatatu (Mei 08) tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo keshokutwa Jumatano (Mei 10) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam saa kumi jioni, kisha itakwenda Afrika Kusini Mei 17, kwa ajili ya Mchezo wa Mkondo wa Pili.
Habari kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa Marumo wameanza safari ya kuelekea Dar es salaam, baada ya kumaliza mchezo wao wa Ligi Kuu ya dhidi ya Mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
“Marumo Jumatatu (leo) wanatarajiwa kuwa huko Dar, wanatarajiwa kutua hiyo siku tayari kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Young Africans, kama ambavyo unafahamu mchezo ni Jumatano hivyo watakuwa na siku mbili za kujiandaa ambazo ni Jumatatu yenyewe na Jumanne.”
“Pengine Marumo wangewahi kuja Tanzania mapema lakini kumbuka Jumapili walikuwa na mchezo mgumu wa ligi kuu dhidi ya Mamelodi hivyo utaona ni kwa jinsi gani ratiba zao ziliwabana.” Imeeleza taarifa kutoka Afrika Kusini
Marumo Gallant ilifanikiwa kufika Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Pyramid ya Misri, huku Young Africans ikiibamiza Rivers United ya Nigeria kwa ushindi wa jumla wa 2-0.