Wakati mjadala wa uhalali wa bao la kusawazisha la mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Young Africans dhidi ya Lipuli FC ukiendelea, afisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire naye ametoa mchango wake.
Masau Bwire ambaye juzi alizibwa mdomo na wekundu wa Msimbazi Simba kwa timu yake ya Ruvu Shooting kukubali kichapo cha mabao saba kwa sifuri, amesema haoni sababu ya watu kulilalamikia bao la Young Africans kwa kusema lilikua halali.
Masau amesema kwake anaamini bao lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Donald Ngoma lilikua halali, kwani mpira ulivuka mstari wa goli na ndio maana mwamuzi aliamuru mpira upelekwe kati.
“Mimi nimeona mpira ulivuka mstari kabisa, hakuna utata wowote katika bao lile, nashangaa kuona watu wakisema Young Africans walibebwa!
“Ukifuatilia vizuri ule mpira uliopigwa kwa kichwa na Ngoma, utaona dhahir mpira ulivuka mstari, wakati mwingine wabongo wanapenda sana malumbao, na hii inatokana na ushabiki uliokithiri miongoni mwetu bila kuangalia jambo kwa umakini”
“Siwatetei Young Africans, ninasema kile nilichokiona katika mchezo wa jana ambao hata hivyo ulikua mzuri na wa kuvutia, kutokana na kikosi cha Lipuli kuonyesha soka safi ambalo liliwafanya wapinzani wao wasifurukute kabisa”. Amesema Msau Bwire