Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire amezitaka mamlaka za soka nchini Tanzania kurudia bao lililokataliwa na Mwamuzi Msaidizi Khamis Chang’walu, walipocheza dhidi ya Young Africans jana Jumatano (Mei 04), Uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma.
Ruvu Shooting walipata bao dakika ya tano, likifungwa na Sadat Mohamed lakini Mwamuzi wa akiba Chang’walu aliashiria mfungaji alikua ameotea kabla ya kutumbukiza mpira wavuni.
Masau Bwire amesema anaamini Mamlaka za Soka zikitazama tena bao hilo kutakua na tafsiri sahihi ya Mfungaji alizidi ama alikua sehemu sahihi kabla ya kufanya maamuzi ya kutumbukiza mpira wavuni.
Amesema kuna baadhi ya watu ambao wamebobea katika masuala la uamuzi wamepinga Maamuzi ya yaliyochukuliwa dhidi ya Ruvu Shooting kwa kukataliwa bao hilo, lakini bado amesisitiza Mamlaka za soka zinapaswa kujiridhisha na kutoa majibu sahihi.
“Nimekasirika sana kwa sababu sikutegemea tukio kama lile kuamuliwa ndivyo sivyo katika mchezo huu, wakati mwingine unajiuliza hivi kweli tunataka mpira wa Tanzania uendelee mbele ama kuishia hapa tulipo?”
“Ninaziomba Mamlaka za Soka kuhakikisha zinajiridhisha na kutoa majibu sahihi kuhusu uhalali wa bao letu ambalo limekatialiwa hapa Lake Tanganyika Kigoma, pia ninatamani hata zile VAR zilizotumika kwenye mchezo wa Simba SC na Orlando zije hapa kuhakikisha hili, maana ni aibu sana.”
“Kwa sababu kama VAR ingekuwepo na Mwamuzi angekubali kwenda kulitazama hili tukio, nina uhakika tulikua tunaondoka na ushindi hapa wa zaidi ya bao moja.” amesema Masau Bwire
Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinakamilika Ruvu Shooting iliyokua mwenyeji ilishindwa kuondoka na Ushindi na kujikuta ikigawana alama na Young Africans inayoendelea na Rekodi yake ya kutopoteza msimu huu 2021/22.