Ushindi wa Simba SC dhidi ya Mbeya Kwanza FC umeendelea kuwa gumzo miongoni mwa wadau wa soka nchini huku wengine wakiamini ulikua halali wengine wakisisitiza haukua halali kwa kisingizio cha Meddie Kagere alikua ameotea.
Simba SC ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo huo wa mwisho wa Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22 jana Jumapili (Februari 06), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Masau Bwire ambaye ni Afisa habari wa Ruvu Shooting ni sehemu ya wadau wa soka nchini waliotoa maoni yao kuhusu ushindi wa Simba SC dhidi ya Mbeya Kwanza FC.
Masau ambaye alikua sehemu ya watazamaji waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa kushudia mchezo huo amesema: “Nishukuru kwamba mpira umekwisha salama, mshindi amepata ushindi ambao pengine alistahili au ameupata kwa bahati bahati, wanajua wenyewe.”
“Kwa ujumla mchezo ulikua mgumu na huu ndio ushindani tunaouhitaji kwenye ligi yetu, na umefika wakati kwa watanzania kufahamu kuwa soka halina mwenyewe, ile tabia ya watu kuamini kwamba timu fulani ni lazima ipate matokeo ikicheza na timu fulani, inapaswa kupuuzwa na watambue mchezo wa soka una tabia ya kutoa matokeo ya kushangaza sana.”
“Umefika wakati wa watu kujua kwamba tunakwenda kuangalia mpira uwanjani na timu yetu itashinda kwa uwezo wake na sio kwa njia za panya, tukienda kwa historia kwamba sisi ni timu fulani tuna asilimia zote za kupata ushindi, matokeo yake ndio unakuta watu wanapoteza fahamu ama kupoteza maisha.”
Kwa ushindi wa bao 1-0 Simba SC inafikisha alama 31 zinazowaweka katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Mbeya Kwanza ikishika nafasi ya 12 ikiwa na alama 13.