Licha ya kuanza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Afisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire, ametamba kwa kutambulisha kauli mbiu mpya ya klabu hiyo kwa msimu huu 2020/21.

Masau amesema msimu huu ambao wameanza kwa sare ya bila kufunga dhidi ya Mtibwa Sugar na kisha kupoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na Ihefu FC, amesema wataitumia kauli mbiu ya ‘KUPAPASA NA KUKUNG’UTA’ kama morari kwa wachezaji wao kupambana vilivyo.

Msimu uliopita alitambulisha kauli mbiu ya ‘MPAPASO SQUARE’ ambayo iliwasaidia kwa kukiwezesha kikosi chao kusalia kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu.

“Kama ambavyo watanzania wanavyotutambua kuwa sisi ni ‘Barcelona ya Bongo’ hivyo wapinzani wetu wajiandae maana tutawapapasa na kuwakung’uta.”

“Tumefanya usajili bora wa kikosi chetu na tunajivunia kwa kuwa wachezaji wetu ni wazawa na kocha pia ni mzawa, hatuna presha na msimu huu tutafanya vizuri hiyo ndiyo imani yetu.”

“Mashabiki waendelee kutupa sapoti kwani kila kitu kinakwenda kwa mpangilio mzuri tutatoa burudani kwa mashabiki kama ilivyo falsafa yetu,” Amesema Masau.

Mwishoni mwa juma hili kikosi cha Ruvu Shooting kinachonolewwa na kocha Charles Mkwasa, kitacheza nyumbani kwa mara ya kwanza msimu huu kwa kucheza dhidi ya Gwambina FC.

UNYAMA: Wasichana wawili wabakwa na genge la wanaume 10
Bares: Dodoma Jiji FC walituzidi