Aishi Manula kuzungumza ukweli kuhusu *Mjigoli* aliofungwa na Bernard Morrison kumeibuka mjadala mitandaoni wenye mitazamo tofauti, wengine wakimpongeza kwa ukweli huo, wengine wakimshutumu, kwa nini aseme hivyo.
Simba na Yanga ukisema kweli ni dhambi, ili uonekane mwema, ukweli hufanye uongo, uongo uwe ukweli, ukisema ukweli, utaitwa msaliti, mamluki, wewe ni wa kule, unafanya makusudi ili uende kule, usipokuwa chonjo, vilago utafungashiwa!
Nilitarajia, kwa kauli ile ya ukweli, aliyoisema Manula kuhusu goli alilofungwa na Morrison, apongezwe na wadau wote kwamba, amekomaa kisoka, na huo ndio uungwana, ( fair play) katika mchezo huu wa kiungwana.
Naamini kila mdau wa soka, aliliona goli la Morrison, aliishuhudia kasi ya mpira kutoka mguuni mwake, hivi kweli, kama ni wakweli, binadamu gani wa kawaida angeweza kujaribu tu kuufuata ule mpira, ukiona kipa yeyote anaufuata na kuuokoa mpira wa vile, huyo siyo wa kawaida, amechanganya ushetani, maana ule mchomo ni hatari, Mungu haruhusu mtu wake kutumbukia dhambini kwa kukifuata kitu hatari kwa afya na uhai, shetani pekee, mwenye kufurahia kifo cha aibu, atakutuma kufanya mambo kama hayo, ufe ili baadaye ashangilie na kukucheka!
Manula anayo maarifa mengi, maarifa hayo, yalimuongoza na kumzuia kuufuata ule mpira, maana angethubutu, angeangamia, mlitaka aangamie wakati yeye maarifa ya kumuokoa anayo? Mwenyezi Mungu anasema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Manula aliyatumia vema maarifa ili kujiokoa na mshuti ule, anastahili pongezi.
Ushabiki wa kugeuza ukweli kuwa uongo, na uongo kuwa ukweli, eti kwasababu unalinda heshima ya timu yako ni wa kishamba, tuuache. Kwa ukweli wa kweli, utaaminika na kuheshimika sana.
Hivi, Manula mlitaka asemeje, ” goli la kawaida, niliteleza tu kwasababu ya utelezi uliokuwepo golini, la sivyo, kimkwaju kile, cha kitoto kabisa, ningekidaka tu, tena kwa mkono mmoja”, angedharaulika sana!
Tumpongeze sana Manula, ameonesha ukomavu kisoka, ameitendea haki fair play, anastahili kupewa tuzo kwa ukweli aliousema kwani, amejijengea heshima, timu yake ya Simba na TFF kwamba ni *WAUNGWANA* katika soka.
Viva Manula…..
Masau Kuliga Bwire – Mzalendo.