Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema vitambulisho vya Taifa vipo mbioni kutolewa baada ya kukamilika kwa mchakato wa makubaliano kati ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kampuni ya utengenezaji wa kadi hizo.
Masauni ameyasema hayo leo Juni 8, 2022 wakati akiongea na wananchi wa Biharamuro mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuelezea malalamiko kuhusu kukosekana kwa vitamabulisho hivyo kwa wengi na kwamba mchakato wake umechukua muda mrefu.
“Wananchi wamekuwa wakilalamika sana na hasa maeneo ya mipakani lakini jitihada za Rais zinaonekana kwani ametupatia pesa ili kukamilisha vitambulisho, na tayari NIDA imesaini mikataba na kampuni yenye tenda ya utengenezaji wa kadi hizo,” amesema Masauni.
Amesema Wizara itahakikisha jambo hilo linamalizika kwa ufanisi baada ya Rais Samia kutoa Shilingi Bilioni 42.5 za kununua kadi ghafi zitakazokamilisha zoezi la utengenezwaji na ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu iliyoanza hii leo Juni 8, 2022.