Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, leo ameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DKT. John Pombe Magufuli akimtaka afike katika ofisi za Kuzuia na kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU, ambapo mapema leo alitia timu ofisini hapo jijini Dodoma kwa mahojiano zaidi.
Amewasili katika ofisi hizo leo Jumamosi Februari 1, 2020 saa 6.17 mchana akitumia gari la uwaziri akiwa amevalia kaunda suti nyeusi.
Alifika dakika 31 tangu Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ramadhani Kailima, kuondoka baada ya kumalizika kwa mahojiano yake na taasisi hiyo nyeti.
Jana Ijumaa, Januari 31, 2020, Takukuru alimuhoji aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola, Meja Jenerali Jacob Kingu (aliyekuwa katibu mkuu) na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye.
Viongozi hao wanahojiwa baada ya agizo la Rais John Magufuli kuitaka Takukuru kuwahoji wale wote waliohusika na mkataba aliodai una harufu ya ufisadi ulioingiwa kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni moja ya Romania ili kununua vifaa mbalimbali vya jeshi hilo.
Magufuli alitoa agizo hilo Januari 23, 2020, wakati akipokea nyumba za Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam ambapo alitangaza kuwafukuza kazi, Lugola na Andengenye na kuridhia ombi la Meja Jenerali Kingu la kujiuzulu.
Katika maagizo yake, Magufuli aliitaka Takukuru kufanya kazi yake ipasavyo bila kujali nafasi ya mtu na kwamba yeyote ambaye angehusika na mkataba huo aliodai ni wa zaidi ya Sh 1 trilioni achukuliwe hatua.