Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema hakuna utaratibu wowote unaoipa mamlaka Jeshi la Polisi kupiga raia au wageni kama baadhi ya askari wanavyowafanyia wananchi bali kuna taratibu za kisheria ambazo zinapaswa kufuatwa pindi raia au mgeni anapovunja sheria.
Hayo yameongelewa leo Mei 08, 2018 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 24 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Ngara Alex Rafael Gashaza ambapo alitaka kusikia kauli ya serikali juu ya kulipa fidia juu ya wananchi wa Ngara na Tanzania kiujumla pindi wanapokamatwa na Polisi, kupigwa na kisha kuja kubainika kuwa hawana hatia.
“Sio utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga raia au hata wageni, kuna utaratibu ikiwa mgeni au raia amevunja sheria anatakiwa uchukuliwe kwa mujibu wa sheria, itabidi tukae tuchunguze kama kuna ukiukwaji wa sheria tuchukue hatua za kisheria ili sheria ifuate mkondo wake”, amesema Mhandisi Masauni.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Masauni amesema pindi hali ya kifedha itaruhusu wanampango wa kukarabati kituo cha Polisi cha Ngara pamoja na nyumba za makazi za maaskari hao.