Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ametangaza kukihama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikiwa ni miaka miwili tangu alipojiunga na chama hicho.
Masha ambaye alihamia chadema katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 amesema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa Chadema imejikita katika kazi ya kukosoa Serikali bila kujiandaa kuwa chama mbadala cha kuongoza baada ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, Masha amedai kuwa Chadema wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kumkosoa Rais John Magufuli binafsi wakati amefanya kazi kubwa na kuyafanyia kazi mambo ambayo viongozi wa Upinzani wamekuwa wakiyalalamikia.
“Sio sahihi kwa vyama vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Mh. Rais John Pombe Magufuli ambaye ni Rais pekee aliyetekeleza kwa vitendo mambo mengi ambayo wapinzani waliyapigia kelele kwa miaka mingi, ikiwemo tatizo kubwa la ufisadi na uzembe katika utumishi wa umma,” Masha ameainisha katika tamko lake.
Hata hivyo, Masha hakueleza wazi kama atajiunga na chama kingine cha siasa baada ya kuitosa Chadema.
Ameeleza ana imani kuwa uamuzi wake huo utampa nafasi zaidi ya kutafakari safari yake ya kisiasa nchini.
Masha ambaye ni mwanasheria kitaaluma, aliwahi kuwa mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza.