Waziri wa zamani wa mambo ya ndani ya nchi, Laurence Masha leo ametangaza kujiengua katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais wa chama cha wanasheria nchini cha Tanganyika Law Society (TLS), unaofanyika wikendi hii jijini Arusha.
Masha amesema kuwa amechukua uamuzi huo kwakuwa anauamini uwezo wa mgombea mwenzake, Tundu Lissu hivyo amewataka wale wote waliokuwa wanamuunga mkono yeye wampigie kura Lissu.
Mawakili nchini kote wamekutana jijini Arusha kwa lengo la kufanya mkutano mkuu wa mwaka unaoambatana na uchaguzi wa kumpata rais wa chama hicho, uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza umekuwa na msisimko mkubwa zaidi na kuzungumziwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Awali, Lissu ambaye alikuwa ameshikiliwa na jeshi la polisi jijini Dar es Salaam na baadae kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya Uchochezi, aliachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 na kufanikiwa kusafiri kwa ndege ya kukodi hadi jijini Arusha ambapo aliingia katika mkutano wa TLS.
Masha na Lissu, wote ni wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mawakili wanachama wa TLS, hali iliyotafsiriwa na baadhi ya watu kuwa uamuzi wa Masha umeshawishiwa na uhusiano wao wa kisiasa.
Hivi karibuni, Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe aliitahadharisha TLS akiitaka kutoingiza siasa katika uendeshaji wake na kutishia kuifuta endapo itafuata mkondo huo.