Serikali imetangaza idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia Uwanja wa Taifa kushuhudia Mtanange wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu Simba SC dhidi ya Young Africans Jumapili.
Miamba hiyo ya soka nchini inakwenda kukutana mwishoni mwa juma hili, baada ya kushinda michezo ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho juma lililopita, ambapo kwa upande wa Simba SC waliibamiza Azam FC mabao mawili kwa sifuri, huku Young Africans wakiifunga Kagera Sugar mabao mawili kwa moja.
Akizungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Taifa, Dar es salaam leo mchana Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini Yusuph Singo amesema MASHABIKI watakaoruhusiwa kuutazama mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya Nusu Fainali, Julai 12 ni 30,000.
Singo amesema sababu ya kufanya hivyo ni kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
“Serikali ilitoa agizo kwamba kwenye mechi zenye uwezo wa kuchukua mashabiki wengi lazima mashabiki waingie uwanjani nusu kwa kuwa Uwanja wa Taifa una uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 basi nusu yake ni 30,000.” Amesema Singo.
Singo ameongeza kuwa Mashabiki pia watapaswa wafuate kanuni za afya ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya Corona.
Taratibu hizo ni pamoja na kuvaa barakoa wakati wa kwenda uwanjani, kunawa mikono kwa maji tiririka na kukaa umbali wa mita moja.