Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeruhusu Mashabiki 60,000 kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa Robo Fainali Mkondo wa Kwanza Kombe la Shirikisho Barani huo kati ya Simba SC dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo Jumapili (April 17), Uwanja hapo, baada ya kutinga Robo Fainali kwa kishindo kwa kuichapa USGN ya Niger mabao 4-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi D, Jumapili (April 03) jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotumwa nchini Tanzania Kupitia Shirikisho la Soka ‘TFF’ imeeleza kuwa, Simba SC itakuwa na fursa ya kushuhudiwa na Mashabiki 60,000 katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa.

Hii ni mara ya kwanza msimu huu kwa Simba SC kupata nafasi ya kuruhusiwa kuwa na Mashabiki 60,000 katika mchezo wa Kimataifa ulio chini ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Mara zote Simba SC imekua ikiruhusiwa kushuhudiwa na Mashabiki 35,000, ambao ni sawa na nusu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua Mashabiki 60,000 walioketi.

Idadi ya Mashabiki wanaopaswa kuingia Uwanja wa Mkapa na viwanja vingine Barani Afrika imekua ikitolewa kwa namba maalum ili kuepuka maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO 19, ambao unasambazwa kwa njia ya hewa.

Maamuzi ya CAF kuruhusu Mashabiki 60,000 Uwanja wa Benjamin Mkapa huenda yamekuja baada ya Uongozi wa Shirikisho hilo kujiridhisha kasi ya maambukizi imepungua kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Majaliwa aitaka TICTS kuimarisha utendaji kazi
Gambo ataka Bunge kujadili mfumuko wa bei