Mipango na matarajio ya klabu ya Al Ahly ya Misri ya kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa tisa wa barani Afrika, inatarajiwa kupewa nguvu na mashabiki 60,000, ambao wanatarajiwa kufurika kwenye uwanja wa Borg El Arab uliopo mjini Alexandria, siku ya ijumaa.
Klabu hiyo nguli nchini Misri, itakua mwenyeji wa mabingwa wa soka nchini Tunisia Esperance, kabla ya kucheza mchezo wa mkondo wa pili Novemba 09 jijini Tunis.
Esperance watakua wakisaka taji la tatu la klabu bingwa Afrika, baada ya kumaliza katika nafasi ya pili mara nne, huku wakikumbuka fainali ambayo walishindwa dhidi ya Al Ahly mwaka 2012, kwa kufungwa jumla ya mabao matatu kwa mawili.
Mshindi wa jumla kwenye mchezo yote miwili ya hatua ya fainali, atakua muwakilishi wa Afrika kwenye michuano ya klabu bingwa duniani, itakayofanyika mwezi Disemba Falme za kiarabu (UAE).
Kwa mara ya mwisho mashabiki wa soka nchini Misri walifanikiwa kuujaza uwanja Borg El Arab mwaka 2012, ambapo mashabiki zaidi ya elfu 65 waliingia uwanjani kushuhudia mchezo kati ya timu ya Misri dhidi ya DR Congo.
Uwanja wa Borg El Arab unachukua mashabiki 86,000, lakini shirikisho la soka barani Afrika “CAF” limezuia mashabiki wasizidi 60,000 uwanjani hapo, kushuhudia mchezo wa mwishoni mwa juma hili kwa sababu za kiusalama.