Mashabiki wa Chelsea wameanza kupata wasiwasi wa timu yao huenda ikaingia kwenye vita kubwa ya kujinusuru kushuka daraja baada ya kuchungulia ratiba ya mechi zao zinazofuata.
Chelsea mwendo wao wa kutopoteza kwenye mechi nne zilizopita ulikoma Jumamosi (Oktoba 28) wakati walipokubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao wa London, Brentford uwanjani Stamford Bridge.
Matokeo hayo yameifanya Chelsea kushika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imeshinda mechi tatu tu kati ya 10 za mwanzo.
Mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi kutokana na ratiba yao ijayo. Baada ya kumalizana na Blackburn Rovers usiku wa leo Jumatano (Novemba Mosi) kwenye Kombe la Ligi, Chelsea itasafiri kwenda kuwavaa vinara wa ligi, Tottenham, Jumatatu (Novemba 06).
Siku nne baadaye, watacheza na Manchester City, kabla ya kwenda St James’ Park kukipiga na Newcastle United. Kisha watarudi Stamford Bridge kucheza na Brighton, Desemba 3 kabla ya saa 72 baadae, kucheza na Man United.
Shabiki mmoja alisema: “Inaweza tusishinde mechi yoyote hapo.”
Mwingine aliandika: “Vita ya kutoshuka daraja inapoanza.”
Shabiki wa tatu aliandika: “Brighton na United ndiyo pekee nadhani tunaweza kuwa na nafasi ndogo, lakini hizo nyingine tusahau.”