Mashabiki wa Liverpool walizomea kama ilivyotarajiwa wakati wimbo wa taifa unapigwa kumpa heshima Mfalme mpya wa taifa la Uingereza aliyesimikwa Jumamosi (Mei 06) Mfalme Charles wa Tatu.
Mamlaka ya Ligi Kuu ya England ilikuwa imewasiliana na klabu tano wenyeji kwenye mechi za ligi hiyo Jumanosi (Mei 06) wakishauri upigwe wimbo wa “Mungu mlinde mfalme” kabla ya kuanza kwa mechi.
Liverpool walijibu kuwa wangetekeleza agizo hilo ingawa walitahadharisha kuwa baadhi ya mashabiki wake wana msimamo mkali juu ya jambo hilo.
Walizomea katika dimba la Anfield wakati wimbo huo unapigwa katika mchezo wao dhidi ya Brentford ambao Liverpool waliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mwaka mmoja uliopita walizomea wakati wimbo huo unapigwa kwenye mchezo wa fainali wa kombe la FA na kwenye kombe la Ngao ya Jamii Julai. Mashabiki wengine wa timu hiyo walitii wimbo huo.
Tottenham walionesha mubashara tukio la kusimikwa kwa Mfalme Charles wa Tatu kwenye Luninga kubwa nje ya uwanja wao kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace.
Wachezaji na waamuzi wa mechi hiyo walikusanyika katikati ya uwanja wakiimba wimbo wa “Mungu mlinde Mfalme”. Sawa na ilivyokuwa kwenye Uwanja wa Etihad wakati wa mchezo baina ya Manchester City na Leeds United.