Mashabiki wa soka mkoani Mtwara wanahofia kudhuriwa na viumbe vikali wakiwemo nyoka, kutokana na kukithiri kwa vichaka katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani humo, licha ya wamiliki kupata mapato yanayoweza kusaidia kuboresha mazingira.
Wakizungumza na Azam TV, mashabiki hao wamesema ni jambo la aibu kwa mkoa wenye rasilimali nyingi kuona uwanja wake unaendelea kuwa na vichaka na kushindwa kuuendeleza tangu wakati ukiitwa ‘Uwanja wa Umoja’ mpaka sasa huku sehemu kubwa ya uwanja huo ukinakishiwa na uchakavu.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara ambao ni wamiliki wa uwanja huo, Zakaria Said, amesema chama hicho kina mikakati ya kuuendeleza uwanja huo lakini amewataka wadau na wapenzi wa soka mkoani Mtwara kujitokeza kuchangia uendelezwaji wa uwanja huo.
Zakaria amesema chama hicho pekee hakina uwezo wa kufanya kila kitu kwani tayari kimekwishafanya ukarabati wa sehemu ya kuchezea iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 100, hivyo wamewataka wananchi wa Mtwara kujitolea kuboresha maeneo mengine.
Uwanja wa Nangwanda Sijaona ndiyo unaotumiwa na Timu ya Ndanda FC kwa mechi zake za nyumbani katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Uwanja huo uliamuliwa kuitwa jina la hayati Nangwanda Sijaona ambaye alikuwa ni moja kati ya wadau wakuu wa maendeleo katika Mkoa wa Mtwara ikiwa ni sehemu ya heshima na kumbukumbu.