Kocha mkuu wa Ndanda FC Meja Mstaafu Abdul Mingange ameonyesha kuchukizwa na tabia za baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo ya mkoani Mtwara ya kuwatusi wachezaji wake wanapokua uwanjani katika majukumu ya kusaka point tatu muhimu.
Mingange ambaye jana alikiongoza kikosi cha Ndanda FC kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting, aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mpambano huo uliochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, hapendezwi na tabia za baadhi ya mashabiki kuwatusi wachezaji wake ambazo zimevuka mipaka.
Mingange alisema ni vigumu kwa kocha kusitisha tabia hiyo, lakini wakati mwingine kwa kusema kupitia vyombo vya habari huenda ikasaidia kwa mashabiki kuhimizana kuacha tabia ya kuwatolea maneno mazito wachezaji wa Ndanda FC.
Alisema umefika muda kwa mashabiki wa soka mkoani Mtwara kubadilika na kuangalia umuhimu wa kuwa na timu ya ligi kuu, hasa katika kipindi hiki ambacho Ndanda FC inahitaji ushirikiano wa hali ya juu ili wafanikishe mpango wa kubaki kwenye ligi hiyo.
“Unapomtusi mchezaji akiwa uwanjani unamvuruga na kuharibu saikolojia yake, haiwezekani kabisa kwa wachezaji wangu kufanyiwa haya wanayofanyiwa, hasa katika kipindi hiki muhimu.”
“Sifurahishwi kabisa na hali hii, maana tunatakiwa kuwa kitu kimoja na hata ikitokea mchezaji anaharibu tunapaswa kufikisha ujumbe kwa njia tofauti na sio kumtukana.” Alisema Mingange.