Sakata la kumshinikiza meneja wa Arsenal Arsene Wenger aondoke Emirates Stadium linalobebwa na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo, limepiga hatua kubwa zaidi, na sasa linaelekea katika mpango wa uwekezaji.
Mashabiki wanaochukizwa na mwenendo wa meneja huyo kutoka Ufaransa na kumtaka aondoke itakapofika mwishoni mwa msimu huu, kutokana na mkataba wake kuelekea ukingoni, wamejipanga kununua hisa za muwekezaji mkuu Stan Kroenke ambaye anadaiwa kumpa jeuri Arsene Wenger.
Wakizungumza na vyombo vya habari jijini London, mashabiki hao wamesema umefika wakati wa kuhimizana wao wenyewe ili kujichangisha fedha ambazo wanaamini zitatosha kununua hisa za muwekezaji huyo ambaye ni mfanyabiashara mkubwa kutoka nchini Marekani.
Mashabiki hao wamepanga kujichangisha fedha hizo na kufikia Pauni milioni 904, ambazo wanaamini zitatosha kununua hisa za muwekezaji huyo, anaedaiwa tangu alipotua klabuni hapo hakuna jambo kubwa alilolifanya zaidi ya kumpa jeuri Arsene Wenger kwa kumuhimiza aendelee kubaki madarakani.
Hata hivyo mashabiki hao wa Arsenel wamesisitiza kuwashirikisha mashabiki wenzao duniani kote kuchangia sehemu ya fedha wanazozikusudia, ili kutimiza lengo lao ambalo wanaamini litakua njia sahihi ya kumng’oa babu huyo alianza kukinoa kikosi cha Arsenal mwaka 1996.
Arsene Wenger amekua katika wakati mgumu, baada ya mambo kumuendea kombo kwa mismu kadhaa, lakini mwaka huu shughuli imekua ngumu zaidi kwake kutokana na kikosi cha Arsenal kukosa muelekeo katika ushindani wa michezo ya ligi kuu ya England pamoja na kuondolewa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kufungwa jumla ya mabao 10-2 dhidi ya FC Bayern Munich.