Wakati mashabiki wa soka nchini wakisubiri kwa hamu mchezo wa Robo Fainali ya African Super League kati ya Simba na Al Ahly ya Misri, habari njema zaidi ni kuwa, tayari maandalizi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, yamekamilika.

Simba SC itavaana na Al Ahly Keshokutwa ijumaa (Oktoba 20) katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya michuano hiyo utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Dimba hilo lilikuwa katika ukarabati kwa miezi kadhaa ili kukidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na lila la Dunia FIFA.

Miongoni mwa maeneo yaliyokarabatiwa katika uwanja huo ni sehemu ya kuchezea (nyasi), majukwaa, taa mpya, vyumba vya kubadilishia kwa wachezaji pamoja na eneo la waandishi wa habari.

Meneja wa Uwanja huo, Milinde Mahona amesema mashabiki wa soka nchini wanapaswa kuwa na amani, kwani tayari maandalizi yote muhimu kwa mchezo huo yamekamilika.

Mahona amesema hali ya uwanja hivi sasa ipo vizuri kwani maboresho yote yaliyotakiwa yamefanyika kwa wakati.

Meneja huyo amesema tayari uwanja huo upo tayari kutumiwa kwa ajili ya mchezo huo wa aina yake utakaoanza saa 12:00 jioni.

“Niwatoe hofu Watanzania, uwanja wetu umekamilika kwa asilimia 100 na upo katika viwango vya CAF na FIFA, umekuwa uwanja wa kisasa, kila mtu ambaye atapata nafasi ya kushuhudia mchezo huo ataona jinsi gani uwanja wetu umebadilika na naamini wageni wetu watafurahia zaidi,” amesema.

Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema shirikisho lipo tayari kupokea ugeni mzito kutoka CAF na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa ajili ya ufunguzi wa michuano hiyo.

“Marais wote vyama na mashirikisho ya soka Afrika watakuwepo, sekretarieti ya CAF itakuwepo, maofisa wakubwa wa FIFA watakuwepo hapa, hivyo ni msafara wa zaidi ya watu 200 utakuwepo hapa na wameshaombewa vibali, kwa hiyo Serikali imeshafanya maombi katika hoteli zote kubwa na zimeshajaa kwani wageni hao wameanza kuingia tangu jana na wangine wataingia kesho,” amesema Ndimbo.

Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa CAF, Patrice Motsepe.

Infantino, Motsepe kuwasili Dar es salaam
Taarifa utekelezaji REA III mzunguko wa pili yapokelewa