Mchekeshaji Kevin Hart jana aliyazua na kuwagawa mashabiki wake baada ya kuporomosha lugha chafu dhidi ya Rais wa Marekani, Donald Trump.
Hart alifyatuka alipokuwa akikabidhi tuzo ya kwanza kwenye kilele cha Tuzo za Video za MTV (MTV – VMAs), tuzo iliyokwenda kwa Tiffany Haddish.
Ilionekana wazi kuwa Hart alikuwa amejipanga kumshambulia Rais Trump kwenye jukwaa hilo, kwani alianza kwa utangulizi kuwa hakuna anayejua nini kinachofuata kwenye show hiyo na kwamba lugha kali zinaweza kutumika.
Baada ya kutumia lugha chafu, ambayo tumeshindwa kuiweka hapa, aliongeza kwa lugha nyingine ya ukakasi ambayo inaonesha kumlenga pia Trump ambaye amekuwa kwenye mgogoro na wachezaji wa kikapu maarufu nchini humo akiwemo LeBrone James.
“Ninaiangalia hii kama mechi ya mpira wa kikapu. Lakini msiwe na shaka, kwasababu kwenye mchezo huu watu wote mnaruhusiwa kupiga magoti! Mnaweza kufanya lolote mtakalo, kwa sababu hakuna ‘mzungu mzee’ ambaye anaweza kuwazuia. Fanyeni tu!”
Kevin Hart ni rafiki wa wachezaji wengi wa mpira wa kikapu akiwemo LeBrone James, ambaye Trump amekuwa akijibishana naye kwenye Twitter. Hivi karibuni Trump alimuita mchezaji huyo kuwa ni ‘mtu mjinga’ baada ya kusikiliza mahojiano yake redioni. Trump alidai kuwa mtangazaji aliyekuwa anamhoji LeBone ndiye aliyefanya aonekana kama ni mtu mwenye akili wakati sio hivyo.
Hata hivyo, ucheshi huo wa Hart kwenye tuzo hizo umesababisha mashabiki ambao wanamuunga mkono Trump kuahidi kutoangalia tena vipindi au filamu zake. Wamedai pia kuwa alitumia maneno ya kibaguzi.
“Hatutaendelea kuangalia tena vipindi vya Kevin Hart kama TKO. Alikuwa mbaguzi kwenye tuzo za jana na alimkosea heshima Rais na watu wote weupe. Lakini nina uhakika ni ‘watu weupe’ ndio waliomkodi kwa ajili ya kutengeneza filamu na show za CBS TV. Lugha hizo za chuki zitaenda naye chooni na vipindi vyake vya TV.” Inasomeka Tweet moja, na nyingine nyingi zilizoponda.
Hart hakuwa mtu pekee aliyeonesha kumpinga Trump kwenye tuzo hizo. Ryan Tedder aliyepanda jukwaani na Logic kutumbuiza alikuwa amevaa fulana inayopinga sera ya Trump ya kujenga ukuta kwenye mpaka wa Mexico. Pia, alisikika akipinga sera ya kuwatenga wakimbizi akisema kuwa Marekani inawakaribisha wote.