Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wameombwa kusahau yaliyopita ili kujenga umoja na mshikamani ili kuhakikisha wanaanza kwa ushindi kwenye Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Ombi hilo kwa Mashabiki na Wanachama limetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipozungumzia mipango na mikakati ya kuelekea kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi msimu huu 2023/24.
Simba SC inatarajiwa kuwa mwenyeji wa ASEC Mimosas Novemba 25 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam na tayari wachezaji wote wameanza mazoezi baada ya mapumziko ya siku tano isipokuwa wale walioitwa kwenye timu za taifa.
Try Again amesema anajua machungu na kejeli wanazokumbana nazo Wanachama na Mashabiki wao kutokana na kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao Young Africans, lakini wanapaswa kusahau na kuendelea kuisapoti timu yao.
“Hiki ni kipindi cha kusahau yaliyopita na kuunganisha nguvu kwa ajili ya michuano inayotukabili kwani ili lengo letu litimie lazima tuwe pamoja na kuendelea kuisapoti timu yetu kwa kuwapa moyo wachezaji wapambane na kupata ushindi dhidi ya ASEC Mimosas,” amesema Try Again.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kampeni na hamasa kuelekea kwenye mchezo huo zitaanza wiki hii huku akiwataka Mashabiki na Wanachama kuachana na kile kilichotokea Novemba 5 na kuelekeza nguvu kuisapoti timu kwenye mchezo huo.
Aidha, Ahmed amesema kabla ya kuivaa ASEC Mimosas wanatarajia kumtambulisha kocha mwenye viwango vya kimataifa atakayerithi mikoba ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’.