Wakati kikosi cha Simba SC kikiwasili salama nchini Botswana tayari kwa kuwavaa Jwaneng Galaxy katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika , Mabosi wa klabu hiyo wamewahakikishia Mashabiki na Wanachama kurejea kwa furaha baada ya kutua Kocha Mkuu Mpya, Abdelhak Benchikha.
Kocha Benchikha raia wa Algeria amechukuwa nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye aliondolewa klabuni hapo baada ya kipigo cha 5-1, kutoka kwa Young Africans mwanzoni mwa mwezi Novemba.
Kocha Benchikha ameweka wazi kwamba yuko tayari kufanya kazi na mchezaji yoyote yule ambaye atajituma na kufanya vizuri na ndio maana anajipa muda wa kumuangalia kila mchezaji nini anakifanya katika nafasi anayoicheza, lakini akizingatia suala la nidhamu ni mkali kwa anayekiuka taratibu anazoziweka kikosini.
“Mimi ni mpambanaji siogopi changamoto ya aina yoyote ile, mchezaji anayejituma nitafanya naye kazi najua sasa hivi timu inapitia kipindi kigumu naamini kwa pamoja tunaweza kuirejesha katika hali nzuri,” alisema Benchikha
Hata hivyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah Try Again’ amesema viongozi wana imani kubwa na Kocha huyơ na ndio maana wamemleta kuinoa timu yao.
Try Again amesema kwa sasa Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kuiunga mkono timu yao, kwa vile mambo matamu yanarudi baada ya kutibuka hivi karibuni hasa baada ya kipigo cha Young Africans.
“Tumeongea muda mwingi na kocha wetu, tumemuahidi kumpa ushirikiano wa asilimia 100 kuhakikisha timu inafanya vizuri,” amesema Try Again aliyeongeza kuwa, wanatambua Mashabiki wao hawana furaha na timu yao kutokana na aina ya matokeo ambayo wanayapata akikiri ni kipindi cha mpito tu.
“Hata kocha tumemwambia ajitahidi kuhakikisha mamilioni ya Mashabiki wetu wanapata kile ambacho wanakihitaji kukiona katika timu yao.” amesema